MBINU MUHIMU ZA KUKUSAIDIA KUSIMAMA IMARA,WAKATI MAMBO YAKO YANAPOKWENDA VIBAYA.


Pamoja na kujihisi kukata tamaa huko, lakini kwa bahati mbaya maisha huwa hayasimami wala kukusubiri mambo yako yawe mazuri, maisha daima huwa yanasongambele. Ni kipindi ambacho huwa unatakiwa kusimama imara na kutuliza akili yako ili uweze kufanikiwa tena. Katika makala ya leo tutakwenda kujifunza mbinu muhimu za kukusaidia kusimama imara, na kuweza kusonga mbele hata mambo yako yanapokwenda hovyo.

Zifuatazo Ni  Mbinu Muhimu Za Kukusaidia Kusimama Imara, Wakati mambo  Yako Yanapokwenda Vibaya. 

1. Jifunze kukubali ukweli wa mambo.
Ni ukweli mambo yako yameshakwenda hovyo na pengine hukutegemea kama hili hiyo inaweza kukutokea, kitu pekee unachotakiwa kujifunza ni kukubali ukweli wa mambo kuwa ndivyo ilivyo. Hutakiwi kujilaumu wala kulalamika sana, kubaliana na hali halisi kisha panga mikakati maalumu ya kuweza kukutoa pale ulipo na kukufanya uweze kusimama imara zaidi katika kipindi hiki ambacho mambo yako hovyo.


  

2. Tambua hiyo hali ipo kwa muda tu.
Huu ndio ukweli unaopaswa kuujua mapema ili kuweza kusimama imara wakati mambo yako yanapokwenda vibaya. Acha kukata tamaa na kuzidi kuumia bila sababu, hakuna tatizo ambalo unaweza kukaa nalo milele kwako. Kila kitu huwa kinakuja na kupotea. Hata tatizo unaloliona kubwa kwako leo, litapita na mambo yatakuwa safi. Kikubwa, jipe moyo na uwe na subira, kisha chukua hatua, utashinda.


3. Chukua jukumu la kusonga mbele bila kukata tamaa.
Mambo yako kukuendea vibaya isiwe kwako ni sababu ama kisingizio cha kukufanya ukashindwa kusonga mbele. Wakati bado pengine unasikilizia maumivu ya mambo yako kukuendea vibaya, kumbuka usije ukaachia ndoto zako zikayeyuka. Ng’ang’ania ndoto na malengo yako mpaka kieleweke. Kuwa shujaa na king’ang’anizi mkubwa wa maisha yako, weka mipango mipya kisha songa mbele bila kuzuiliwa na kitu chochote.

4. Jenga fikra chanya zaidi.
Matatizo katika maisha yetu ya kila siku, ni kitu ambacho mara nyingi huwa hakikwepeki hata iweje. Badala ya kukaa na kuanza kuumia na kujilaumu zaidi, jifunze kuwa na mtazamo chanya. Weka mikakati yako vizuri ya kutoka hapo tena, acha kuongelea sana matatizo yako na chukua hatua sahihi za kukabiliana na tatizo lako. Kwa kadri jinsi utakavyokuwa na mtazamo chanya ndivyo utakavyozidi kuona mwanga wa mafanikio kwako.


5. Jifunze kutatua tatizo lako kwa hatua.
Acha kuumiza kichwa kwa kutaka kuona tatizo lako unalitafutia njia sahihi na kuisha mara moja. Jipe muda na litatue pole pole na mwisho wa siku litaisha. Kama utaendelea kukaa na kufikiri sana, sasa itakuaje, nitafanyaje, itakuwa ni kwako sawa na kupoteza muda. Chukua hatua, hata kama ni ndogo ndogo ambazo zitakuletea majibu chanya ya tatizo linalokusumbua na mwisho utafanikiwa. 


6. Kuwa na shukrani kwa kidogo ulichonacho.
Natambua ni hali inayoweza kuwa inakukatisha pengine tamaa kutokana na mambo yako kukuendea vibaya. Lakini kumbuka hujakosa kila kitu katika maisha yako. Jifunze kuwa na shukrani kwa kile hata kidogo ulichonacho. Jaribu kukaa chini na kujiuliza nini ulichonacho ambacho unaweza ukajivunia ingawa mambo yako hayako vizuri. Inawezekana ukawa unakipaji kizuri, shukuru hata kwa hilo badala ya kulalamika.

Ili uweze kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa uliyojiwekea katika maisha yako ni muhimu sana kwako kung’ang’ania na kushikiria mipango na malengo yako hata katika kipindi ambacho mambo yako hayako vizuri. Acha kukata tamaa, jipe moyo, kisha songa mbele kwa hali yoyote uliyonayo. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo yanayoweza kukusaidia kusimama imara kipindi ambacho mambo yako yanapokwendea vibaya.

     Nakutakia Mafanikio Mema.


Designed by CHAX C

Comments