SABABU ZA MOYO KUPANUKA NA MATIBABU YAKE.

Moyo kupanuka au kuwa mkubwa ni tatizo ambalo huathiri utendaji wa mfumo wa usambazaji damu mwilini. 

Ni hali inayosababishwa na ukinzani wa moyo jinsi unavyotoa na kuingiza damu katika mishipa ya moyo na kuelekea sehemu mbalimbali za mwili. 

Moyo kupanuka kutokana na kutokana na mazingira ya kusukuma damu kwa nguvu ya ziada tofauti na kawaida, hivyo kusababisha misuli ya moyo kuharibika. Wakati mwingine moyo hutanuka bila sababu zinazojulikana moja kwa moja. Pia, wakati mwingine moyo unaweza kutanuka kwa kipindi kifupi kutokana na mgandamizo kwenye mwili wako mfano ujauzito. 

Hali nyingine ni tatizo la moyo ulilozaliwa nalo, kuharibika kwa moyo kutokana na mshtuko wa moyo, kudhoofu kwa misuli ya moyo au moyo kutodunda kwa mpangilio. Mazingira hayo huweza kusababisha moyo kutanuka. 

Hali zingine za kiafya zinazohusiana na moyo kutanuka ni kama zifuatazo: 
Kupanda kwa shinikizo la damu. Hali hii husababisha moyo kusukuma damu kwa nguvu zaidi ili kuifikisha sehemu mbalimbali za mwili. Hali inayosababisha misuli ya moyo kutanuka na kuwa minene hivyo kufanya moyo kuongezeka ukubwa. 

Kupanda kwa shinikizo la damu kunaweza kusababisha ventrikali ya kushoto kupanuka na kufanya misuli ya moyo kudhoofika. Shinikizo la juu la damu pia hufanya sehemu ya juu ya moyo kutanuka. 

Ugonjwa wa misuli ya moyo Ugonjwa huu husababisha misuli ya moyo kukakamaa na kusababisha moyo kujaribu kusukuma damu kwa nguvu zaidi kitu kinachoweza kusababisha moyo kutanuka. 

Kupanda kwa shinikizo la damu kwenye mshipa wa damu unaounganisha moyo na mapafu Hali hii hujulikana kitaalamu kama Pulmonary Hypertension. Hii husababisha moyo kusukuma damu kwa taabu kwenda na kutoka kwenye mapafu ambako huwekewa hewa ya oksijeni. 

Hali hii husababisha upande wa kulia wa moyo kutanuka au kuwa mkubwa. 
Kuwapo maji kuzunguka moyo Maji kukusanyika kwenye mfuko unaobeba moyo, huweza kusababisha kuonekana mkubwa hasa baada ya kupiga picha ya x-ray. 

Upungufu wa damu mwilini Kuwa na kiwango cha chini cha chembe hai nyekundu za damu hufanya ubebaji mdogo wa oksijeni kwenda sehemu mbalimbali za mwili, husababisha moyo kutumia nguvu nyingi kusukuma damu kwa haraka ili kuweza kusambaza oksijeni ndogo kwa haraka itosheleze mahitaji. 

Kusukuma huko kwa haraka husababisha moyo kutanuka au kuwa mkubwa. 
Matatizo ya tezi. Ikiwa tezi zinatoa homoni kwa kiwango kikubwa au kidogo, husababisha matatizo ya moyo yanayojumuisha utanuke na kuwa mkubwa.

Kuwapo kwa wingi wa madini chuma mwilini 
Hali hutokea pale mwili unashindwa kutumia madini ya chuma vizuri. Hali hiyo husababisha madini haya kujijenga kwenye ogani mbalimbali za mwili, ikiwa ni pamoja na moyo. 

Kuwapo kwa madini chuma kwenye moyo husababisha kutanuka kwa ventrikali ya kushoto na kuwa sababu ya kudhoofu kwa misuli ya moyo. 

Magonjwa ya moyo kama Amyloidosis 
Ugonjwa huu hutokana na protini isiyo ya kawaida inapozunguka kwenye damu. Protini hiyo ikifika kwenye moyo huweza kuziba baadhi ya mirija hivyo kuingilia utendaji wa kawaida wa moyo na kufanya moyo kutanuka. 

Dalili za Moyo Kutanuka 
Moyo kutanuka huonekana kwa picha ya X-ray ya kifua ingawa vipimo vingine vinahitajika ili kubaini ni nini kinasababisha moyo kutanuka. 

Baadhi ya watu wenye moyo mkubwa hawana dalili za moja kwa moja, ingawa wengi hupata dalili kama kupumua kwa tabu, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kujaa au kuvimba kwa mwili hasa miguu, wakati mwingine vidole kufa ganzi na kukakamaa. 

Dalili nyingine ni kifua kubana au kuuma, kupata kizunguzungu, kuhisi hali ya mwili kunyong’onyea au kutokuwa na nguvu, kupoteza fahamu na kuzimia. 

Moyo kutanuka ni hali ambayo inayoweza kutibiwa kwa urahisi ikiwa itagundulika mapema. Hivyo ni vyema kutafuta msaada wa kitabibu ikiwa unapata dalili za matatizo ya moyo. 

Matibabu 
Matibabu ya moyo mkubwa yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa, kubadili mfumo wa maisha na wakati mwingine upasuaji. Mara nyingi moyo ukipanuka husababisha baadhi ya sehemu kwenye misuli ya moyo kutokufikiwa na damu, hivyo kusababisha tundu kwenye moyo au kidonda cha moyo na baadaye kupooza. 

Kuepuka tatizo hili 
Kuepuka ulaji wa nyama kwa wingi, hasa ile nyekundu, kupunguza matumizi makubwa mayai na maziwa kupindukia. 

Punguza matumizi ya vyakula vya kusindikwa, epuka mafuta yatokanayo na wanyama, tumia yale yanayotokana na mimea kama alizeti, karanga, nazi na mawese, tena kwa kiasi kidogo.

Source:Muungwana

Designed by CHAX C

Comments